1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UgaidiAsia

Watoto wauwawa katika shambulio mjini Peshawar

27 Oktoba 2020

Watoto saba wameuwawa na wengine wengi wamejeruhiwa katika shambulio la bomu kwenye shule moja ya kidini Kaskazini Magharibi mwa mji wa Peshawar. Hakuna kundi lililodai bado kuhusika na shambulio hilo.

https://p.dw.com/p/3kVQO
Pakistan Anschlag auf eine Religionsschule in Peschawar
Picha: Abdul Majeed/AFP/Getty Images

Kulingana na Waqar Azim mmoja wa maafisa wakuu wa polisi mjini humo, zaidi ya watu 60 walikuwa wanahudhuria mafunzo ya kidini wakati bomu liliporipuka katika shule hiyo ya Kiislamu ilioko kilomita 170 magharibi mwa mji wa Islamabad.

Soma pia: Watu 10 wafariki katika shambulizi la soko la hisa Pakistan

Akizungumza na shirika la habari la AFP, afisa huyo amesema bomu lililoripuka lilikuwa limefichwa ndani ya begi lililoachwa darasani humo, huku akiongeza kuwa mtu anayeshukiwa kuliacha begi hilo aliondoka darasani humo kabla ya mripuko huo kutokea katika ukumbi wa chuo cha Jamia Zuberia.

Mohammad Ali Gandapur, ambae ni afisa mwengine mkuu wa polisi, amesema watu saba wameuwawa katika shambulizi hilo huku wengine 50 wakijeruiwa.

Mohammad Asim Khan, msemaji katika hospitali moja ilioko karibu na eneo lilikotokea shambulio amethibitisha mauaji ya watu hao saba na kujeruhiwa kwa zaidi ya watu 70 waliopelekwa katika hospitali hiyo.

Pakistan Anschlag auf eine Religionsschule in Peschawar
Mwanachama wa kikosi cha kutegua mabomu akikagua vifaa vya wanafunzi baada ya mlipuko katika shule mjini Peshawar.Picha: Fayaz Aziz/Reuters

Wengi waliouwawa ni wanafunzi wa kiume kati ya miaka 20 hadi 40. Walimu na watoto walio juu ya miaka 7 ni miongoni pia mwa waliojeruhiwa.

Soma pia: Wapakistan wamaliza kupiga kura licha ya mashambulizi na mauaji

Mwalimu mmoja katika chuo kikuu hicho Safiullah Khan ameliambia shirika la habari la AFP kwamba zaidi ya wanafunzi 1000 wanahudhuria masomo katika chuo hicho cha mafunzo ya kidini kilichogawanywa katika sehemu mbili, moja ya wanafunzi walio zaidi ya miaka 18 na sehemu nyengine ni ya watuto wadogo.

Somo lililokuwa linafunzwa darasani humo lililokuwa linapeperushwa moja kwa moja kupitia mtandao wa kijamii uliomuonesha mwalimu akifundisha, kwa lugha ya Pashto na kiarabu, akielezea hadithi ya mtume Mohammed wakati shambulio lilipotokea.

Soma pia:Taliban na Pakistan kujadili mazungumzo yaliyositishwa

Muda mfupi baadae, wafanyakazi wa uokozi, na wakaazi wa mji wa Peshawar walionekana katika eneo la tukio wakiwasaidia wanafunzi waliojeruhiwa pamoja na kuokota vitabu, viatu na kofia zilizokuwa zimetapakaa kila mahali.

Waziri Mkuu Khan aahidi kuwasaka wahusika

Kwa upande wake waziri mkuu wa Pakistan Imran Khan ametoa salaam za pole kupitia mtandao wa kijamii wa twitter akiandika, "nataka kulihakikishia taifa langu kwamba serikali itahakikisha wale waliotekeleza shambulio hili la kigaidi na kinyama wanafikishwa mbele ya sheria haraka iwezekanavyo."

Pakistan Anschlag auf eine Religionsschule in Peschawar
Wanafunzi wasiopungua saba wamefariki katika shambulio shule ya kidini mjini Peshawar, Oktoba 27, 2020.Picha: Abdul Majeed/AFP/Getty Images

Shambulio hilo lililosikika katika baadhi ya maeneo mjini Peshawar liliharibu kabisa jengo la chuo hicho. Hata hivyo haijajulikana kwa haraka ni kwasababu gani chuo hicho kililengwa, na hakuna mpaka sasa kundi lolote lililojitokeza kukiri kuhusika na tukio hilo ambalo limetokea baada ya miezi kadhaa ya utulivu nchini Pakistan.

Soma pia:Chuki dhidi ya Uislamu: Imran Khan ajenga daraja kati ya mashariki na magahribi

Peshawar imewahi kuwa ngome ya mashambulizi kutoka kwa kundi la wapiganaji wa jihadi wakivilenga vikosi vya usalama na maeneo ya wazi ya mji huo ulio Kaskazini Magharibi mwa eneo linalopakana na Afghanistan.

Matukio ya mashambulio yalikuwa yamepungua katika miaka ya hivi karibuni nchini Pakistan kufuatia msururu wa operesheni za kijeshi karibu na eneo la mpakani lakini makundi ya wanamgambo bado yameweza kuendelea kushambulia.

Chanzo: AFP