Israel yasogeza mbele muda wa kuidhinisha makubaliano
16 Januari 2025Israel imesema wataidhinisha makubaliano hayo hadi pale kundi la Hamas litakapoheshimu masharti yote katika kile ilichokiita "mgogoro wa dakika za mwisho." Netanyahu anasema hayo muda mfupi baada ya Israel na Hamas kufikia makubaliano ya kihistoria ya kusitisha mapigano kwa muda wa wiki sita huko Ukanda wa Gaza pamoja na kuachiliwa mateka, hatua inayoibua sintofahamu juu ya utekelezwaji wa makubaliano hayo.
Soma pia:Makubaliano ya kuvimaliza vita vya Gaza bado yasubiriwa
Makubaliano ya kusitisha mapigano yamefikiwa jana Jumatano, na wapatanishi kwenye mzozo huo wanasema huenda yakafungua njia ya kufikiwa kwa makubaliano ya kudumu ya kuvimaliza vita kwenye Ukanda wa Gaza. Lakini matamshi haya ya Netanyahu yanaibua sintofahamu juu ya utekelezwaji wake, baada ya hapo awali ofisi ya waziri mkuu huyo kulishutumu kundi la Hamas kwa kukiuka baadhi ya masharti ya makubaliano hayo. Hata hivyo haikufafanua zaidi.
Mapema leo, vyombo vya habari vya Israel viliripoti kwamba Baraza la Mawaziri litakaa ili kuyaidhinisha makubaliano hayo.
Kundi la Hamas, lenyewe limesema liko tayari kuyatekeleza makubaliano hayo, hii ikiwa ni kulingana na afisa mwandamizi Izzat el-Reshiq hii leo.
Makubaliano hayo yaliyoratibiwa na Qatar yanajumuisha awamu ya kwanza ya kuwaachilia mateka 33 wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas pamoja na wafungwa kadhaa wa Kipalestina na yanatarajiwa kuanza kutekelezwa Jumapili, siku moja kabla ya kuapishwa Rais mteule wa Marekani Donald Trump, ambaye mjumbe wake katika eneo la Mashariki ya Kati pia alihudhuria mazungumzo hayo yaliyodumu kwa muda mrefu, bila ya kuzaa matunda.
Soma pia:Hatua kubwa katika mazungumzo kati ya Israel na Hamas Doha
Shangwe ziliripuka kote kwenye Ukanda wa Gaza baada ya tangazo hilo. Randa Sameeh rais wa Gaza City alisema anahisi ni kama ndoto, kwamba baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa sintofahamu, hatimaye kila kitu kinafikia mwisho. Akaongeza kuwa wamepoteza ndugu zao wengi na wamepoteza kila kitu.
Rais wa Israel aiomba serikali yake kuyaidhinisha makubaliano hayo
Kundi la Hamas lilisema baada ya makubaliano hayo kwamba, yalikuwa ni matokeo ya msimamo makini wa watu wa Palestina na mapambano waliyoyaonyesha kwenye uwanja wa vita huko Ukanda wa Gaza.
Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu imesema kiongozi huyo jana Jumatano alizungumza kwa njia ya simu na Rais Joe Biden wa Marekani na kumshukuru kwa kusaidia kufikiwa kwa makubaliano hayo, ingawa alisisitiza kwamba bado kuna masuala ya mwishomwisho yanayoendelea kufanyiwa kazi.
Rais wa Israel Isaac Herzog, kwa upande wake amesema makubaliano hayo yalikuwa ni njia muafaka kuelekea kuwarejesha mateka waliokamatwa Oktoba 7, 2023, baada ya wanamgambo wa Hamas kuishambulia Israel, na kuchochea kuibuka kwa vita. Kwenye shambulizi hilo raia 1,210 wa Israel waliuawa na wengine kuchukuliwa mateka na kuitolea wito serikali ya Israel kuyaunga mkono na kuimaliza sintofahamu iliyopo.
Waziri mkuu wa Qatar ambayo ndio mpatanishi mkuu, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim al-Thani amesema usitishaji huo wa mapigano utaanza kutekelezwa Jumapili na kuhusisha kubadilishana mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina. Kisha baada ya hapo masharti ya mapatano mapana ya mpango huo wa amani yatakamilishwa.
Viongozi mbalimbali wa dunia wamepongeza hatua ya kufikiwa kwa makubaliano hayo wakisema inatoa matumaini kwa raia wa pande zote ambao wamepitia mateso makubwa na kwamba yatasaidia kuendeleza juhudi za kufanikisha amani ya kudumu kati ya Israel na Palestina.
Kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei ameupongeza "upinzani" wa Palestina baada ya makubaliano hayo na kusema dunia ilitambua kwamba subira ya watu wa Gaza na msimamo wao umeulazimisha utawala wa Israel kurudi nyuma. Amesema hayo kupitia ukurasa wa X.