1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Makubaliano ya kusitisha vita vya Gaza yanukia

14 Januari 2025

Duru ya mwisho ya mazungumzo ya kusitisha vita vya Gaza yaanza nchini Qatar. Rais wa Marekani Joe Biden pia amesisitiza juu ya kufikiwa makubaliano hayo na kuachiwa mateka wa Israel

https://p.dw.com/p/4p8KX
Israel Gaza-Grenze 2023 | Israelische Artillerie beschießt Ziele im Gazastreifen
Picha: Jim Hollander/Matrix Images/picture alliance

Kuhusu duru hiyo ya mwisho ya mazungumzo inayolenga kuvimaliza vita katika Ukanda wa Gaza, kati ya Israel na Hamas baada ya vita hivyo kuendelea kwa zaidi ya miezi 15, Qatar imesema lengo la mkutano wa leo Jumanne ni kukamilisha vipenegele vilivyosalia kabla ya kuukamilisha mpango huo amani.

Wakuu wa mashirika ya kijasusi ya Israel, wajumbe wa Mashariki ya Kati, wawakilishi wa utawala wa sasa wa Marekani na wale wa utawala ujao na Waziri Mkuu wa Qatar wapo kwenye mkutano huo wa leo.

Baadae wapatanishi wanatarajiwa kukutana pembeni na maafisa wa Hamas.

Marekani | Rais Joe Biden
Rais wa Marekani Joe Biden Picha: Roberto Schmidt/AFP

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel Gideon Sa'ar, amethibitisha kwamba mafanikio makubwa yamepatikana katika mazungumzo yanayoendelea ya kusitisha mapigano Gaza kati ya Israel na Hamas yanayofanyika katika mji mkuu wa Qatar, Doha.

Rais wa Marekani Joe Biden amesema makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na Israel katika ukanda wa Gaza na kuachiliwa kwa mateka yanakaribia kukamilika.

Soma pia: Rasimu ya mwisho ya kusitisha vita vya Gaza yatolewa

Biden, amesema: "Waliotekwa wanastahili kuungana tena na familia zao. Kwa hivyo tunajitahidi ili makubaliano yapatikane. Makubaliano tuliyoyapendekeza yanahusu kuwakomboa mateka, kusimamisha mapigano, kuhakikisha usalama wa Israel na kuruhusu kuongezwa misaada kwa Wapalestina ambao wameteseka vibaya katika vita hivi.”

Wakati huohuo watu wapatao 18 wameuawa katika mashambulizi ya Israel ya usiku wa kuamkia siku ya Jumanne katika Ukanda wa Gaza. Miongoni mwa waliouawa ni wanawake sita na watoto wanne taarifa hiyo ni kwa mujibu wa maafisa wa afya wa Gaza. Maeneo ya Deir al-Balah na Khan Younis ndio yaliyoshambuliwa.

Hata hivyo hakuna tamko lolote kutoka upande wa jeshi la Israel kuhusiana na mashambulio hayo. Israel imesema katika vita vyake inawalenga wapiganaji pekee na imewalaumu wapiganaji hao kwa kujificha miongoni mwa raia katika maeneo au kambi za kuwahifadhi raia.

Ukanda wa Gaza |  Khan Younis
Athari ya vita katika mji wa kusini wa Khan Younis katika Ukanda wa GazaPicha: Mahmoud Fareed/Zuma/picture alliance

Na nchi mbalimbali zitashiriki kuanzia hapo kesho Jumatano katika mkutano wa kimataifa unaolenga kutafuta suluhu juu ya kuanzishwa nchi mbili za Israel na Palestina. Wizara ya mambo ya Nje ya Norway imesema, mataifa kadhaa yatapeleka wajumbe wao nchini humo kushiriki katina kutafuta njia za kuumaliza mzozo huo.

Waziri Mkuu wa mamlaka ya Palestina Mohammed Mustafa, mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA Philippe Lazzarini, na mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa Mashariki ya Kati Tor Wennesland ni miongoni mwa wajumbe watakaohudhuria mkutano huo.

Soma pia: Makubaliano ya kusitisha vita Gaza yakaribia kufikiwa

Utakuwa ni mkutano wa tatu wa Muungano wa Kimataifa wa Utekelezaji wa Suluhu ya Nchi Mbili, ambao kuundwa kwake kulitangazwa mwezi Septemba kandoni mwa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York.

Hata hivyo, wachambuzi wanasema uwezekano huo bado ni mgumu kufikiwa wakati ambapo Israel yenyewe haiungi mkono hatua hiyo.

Vyanzo: AFP/AP/RTRE